Shairi: Dunia Bahari Kuu
Dunia duara, ndivyo asemavyo babu
Katu mie sipingi,anazo sababu
Kwani ina vituko,tena vingi ajabu
Dunia bahari,mja sipige mbizi
Kingo zilizofungaka,mwisho haunekani
Inazo sifa tajika,nzuri na za huzuni
Mara moja tacheka,ghafla ije huzuni
Dunia bahari,mja sipige mbizi
Ina meno makali,zaidi ya msumeno
Yanakata vikali,usibaki hata mkono
Wewe mwenye akili,jiepushe usiwe mfano
Dunia bahari,mja sipige mbizi
Dunia ina madhila,sishindane nayo
Ina chache fadhila,epukana nayo
Siifanyie hila,takutia jongomeo
Dunia bahari,mja sipige mbizi
Ina makali mawimbi,usije ukasombwa
Dunia ni hatari,haitambui mpendwa
Inavyo vingi vitimbi,chunga usije naswa
Dunia bahari, mja sipige mbizi
Dunia gae bovu,lisilo thamani
Imejaa mauvu,haina tena amani
Chunga usiipe shavu,haina shukrani
Dunia bahari,mja sipige mbizi
Kaditama nafika,yanipasa kuondoka
Nasaha hiyo shika,isije tena ponyoka
Usije danganyika,mabaya yakakufika
Dunia bahari,mja sipige mbizi
@Malenga wa bara
*Ayieko Jakoyo*
Ayieko Jakoyo ni mwandishi wa mashairi na makala mengine katika lugha ya kiswahili na kiingereza