Shairi: BADO SIJAFIKA
Na Ayieko Jakoyo
Vina naokoteza, kutunga haba mshororo
Najaribu kueleza, katika lugha nyororo
Bado najikoleza, kwa wa jana uporo
Mie bado kufika, mshairi natapatapa
Sijawa bado malenga,sinivishe cha ukoka
Mie bado mchanga, ndio bado naibuka
Ila najitoa mhanga,ushairi kuandika
Mie bado kufika,mshairi natapatapa
Kama kuku mgeni,ndo kwanza nazoea
Kwenye hii fani,wapo walobobea
Nami natamani,niweze kupepea
Mie bado kufika,mshairi natapatapa
Najua ni matani,mniitapo gwiji.
Sijabobea kindani,ila naomuomba mpaji
Anipe jicho la ndani, akoleze changu kipaji
Mie bado kufika,mshairi natapatapa
Ushairi ni fani,isokuwa na mchezo
Lazima ujue mizani, vipande na kibwagizo
Pia uweze kughani,ujue vingi vigezo
Mie bado kufika, mshairi natapatapa
Kwa jina la Rabuka,napiga langu dua
Niweze ibuka,tungo nzuri kuzitoa
Nisifike Afrika,kwa kazi iso doa
Mie bado kufika,mshairi natapatapa
Kaditama nafika,shukrani mashabiki
Yanipasa kuondaka,ila tubaki marafiki
Hongera kufurika,nyote nawapa tiki
Mie bado kufika,mshairi natapatapa
Malenga wa bara, Ayieko Jakoyo
I see good work